Nimehadithiwa kisa kimoja cha kweli na cha kustaajabisha ambacho kimeniacha na maswali mengi na mwisho nikamuuliza aliyenihadithia; “huyo jamaa hakuwa jini kweli? kisa chenyewe nimehadithiwa na dada mmoja aged between 35 – 40 ambaye hapendi nimtaje jina. Alinihadithia kama ifuatavyo:
Mambo? (naishi nae jirani), nina stori nataka nikupe, maana mimi mwenyewe nimeshangaa na mpaka sasa hivi siamini kilichotokea. Wiki iliyopita nilikwenda Morogoro, wakati naondoka hapa nyumbani (anakaa Ilala) kwenda Ubungo nilichukua teksi. Wakati naondoka nilikuwa na jumla ya shilingi 280,0000.
Nilichukua shilingi 30,000 nikaweka kwenye pochi ndogo kisha nikaweka kwenye sidiria, iliyobaki 250,000 nikaweka kwenye bahasha halafu nikaiweka kwenye mkoba wangu ambao nilipokuwa kwenye teksi, niliuweka kwenye kiti cha abiria cha nyuma.
Huyo dereva huwa namuona tu, kwani gari lake huwa analaza jirani yetu, lakini simjui vizuri. Tukiwa tunaelekea ubungo stendi, nilikumbuka simu yangu, nilipojisachi nikaona sina, lakini nilikuwa na uhakika nilipanda nayo, nikamuomba dereva aipige simu yangu ili kama imeangukia ndani ya gari niione.
Nikampa namba yangu akaipiga, kweli ikaita kutoka chini ya kiti nilichokuwa nimekaa. Nikaiokota kisha nikaiweka vizuri tukaendelea na safari yetu hadi Ubungo, tulipofika nikamlipa dereva nauli yake tukaagana. Mimi moja kwa moja kwenye basi hadi Morogoro.
Nilipofika nyumbani Morogoro, nikafungua mkoba wangu ili nitoe ile bahasha yenye 250,000, lakini sikuiona, nikajaribu kupekua vizuri kila mahali lakini wapi, moja kwa moja nikajua ile bahasha yenye pesa nimeibiwa.
Lakini nilipotafakari vizuri, nakaamini sikuibiwa kwenye basi, bila shaka itakuwa nimeidondosha kwenye teksi wakati naiweka vizuri mara baada ya kutoa zile elfu 30, ambazo nilizitoa ili nisipate shida kutoa hela ya nauli ya basi na kutatua shida ndogondogo za njiani.
Kwakweli nilichanganyikiwa, ukizingatia ndiyo pesa niliyokuwa naitegemea katika biashara yangu niliyoendea huko na sikuwa na hela nyingine. Dereva teksi simjui wala namba yake sina, lakini nikakumbuka nilimpa namba yangu ya simu tukiwa tunaelekea Ubungo ili kuipiga wakati natafuta simu yangu. (angalia mambo yanavyoenda hapa).
Nikachukua kisimu changu, nikaangalia missed call za mwisho na kwa kuwa sikuwa nimepigiwa simu na watu wengi, niliiona namba yake mara moja, nikampigia. Huku roho ikinidunda, dereva akapokea simu na baada ya kujitambulisha kwake akanikumbuka na nikamuuliza kama ameokota bahasha kwenye gari yake!
Dereva teksi akasema hajaiona, ila baada ya kunishusha mimi, alipofika kituo cha daladala kilicho jirani na stendi ya Ubungo kuelekea Posta, alipata abiria wengine wanne (si unajua ule mtindo wa abiria wanne kuchanga buku buku) ambao aliwapakia hadi posta.
Wakati wanaelekea posta, abiria mmoja alimuuliza: “dereva, kuna abiria yoyote alipanda huma kabla yetu,?” dereva akamjibu ndiyo. “Basi naomba nikupe namba yangu, akikupigia, mpe namba yangu anaipigie,” alisema yule abiria ambaye ni mwanume wa makamu kiasi. Hata dereva teksi alipotaka kujua kulikoni, hakuambiwa.
Basi, nikamuomba dereva teksi anitumie ile namba na baada ya kunitumia nilimpigia yule kaka. Baada kumpigia simu iliita na kupokelewa. Nikajitambulisha kwake kisha akaniuliza kiasi cha pesa kilichomo na jina langu, maana kwenye ile bahasha niliweka na kitambulisho changu cha kupigia kura.
Baada ya maelezo mafupi, yule kaka akaniambia niondoe wasiwasi hela zangu zote zipo na kunieleza kuwa mara baada ya kupanda kwenye ile teksi, aliiokota bahasha hiyo chini kwenye kiti cha nyuma na hakumwambia abiria mwingine zaidi ya kumuuliza dereva teksi.
Hivyo akaniambia kuwa yeye anafanyakazi Tanesco Ubungo, nikirudi nimtafute anipe pesa zangu. Nikamwambia nimtume ndugu yangu amtafute popote alipo ili ampe hizo pesa ili mimi jikirudi kutoka Morogoro nizikute nyumbani, kaka akakataa, akasisitiza lazima anikabidhi mimi mwenywe!
Nikakubaliana naye, lakini akili ya kwanza kunijia kichwani nikahisi huu utakuwa ndiyo mwanzo wa kutongozwa, lakini yote namwachia Mungu. Hata hamu ya kukaa Morogoro sikuwa nayo, nikalazimika kugeuza siku ya pili yake kurejea Dar.
Nilipofika Dar, nikampigia simu kumtaarifu kuwa nimesharudi, akaniambia niende Ubungo Bus Stand na nikifika pale nimpigie simu atakuja nilipo, kwani ofisi zake zipo jirani hapo Tanesco Ubungo.
Kwa kuwa sikuwa najiamini, nilifuatana na ndugu yangu mmoja hadi Ubungo, nilipofika nilimpigia simu yule kaka, kwanza simu iliita kwa muda mrefu bila kupokelewa, nikaanza kuingiwa na wasi wasi huenda nimelshaingizwa mjini. Baadae nilipiga tena na kumpata, akaniambia alikuwa msikitini nimsubiri atakuja baada ya muda. Nilikaa tena kwa muda mrefu na kuendelea kuingiwa na wasiwasi zaidi, kwani alikuwa hatokei.
Wakati naanza kukata tama, mara nakaona simu inaita, kuangalia nakaona ni yule kaka, akaniambia ameshafika na ananitafuta. Nilianza kumuona mimi, nikamuelekeza nilipo akaja.
Wakati anakuja, roho ilikuwa ikinienda mbio, sikuwa na uhakika kama kweli ananiletea pesa zangu au kuna dili anataka kunichezea. Maana kwa mji wa Dar, lolote linaweza kukukuta bila kutarajia.
Alipofika, kwanza alituomba samahani kwa kuchelewa na baada ya kutambulishana pale, akanyoosha mkono wake akaniambia: HESABU PESA ZAKO DADA! Huku moyo ukinienda mbio, nikapokea na kuhesabu pesa zangu huku natetemeka. Nikakuta ZOTE ZIKO SAWA, haikupungua senti tano!!!
Na mimi kuonesha uungwana, nikahesabu shilingi 50,000 nikampa. YULE KAKA AKAZIKATAA KABISA, akasema nimpe hela ya teksi tu shilingi 4,000 aliyokuja nayo pale. Sikuamini masikio yangu. Kweli nikampa kisha tukaaga na akaondoka zake. YULE KAKA SIMJUI, HANIJUI!
Kwa dunia tuliyonayo sasa, nashindwa kuamini kama bado tuna watu waamminifu kama huyu kaka. Hakika mtu kama huyu malipo yake ni makubwa hapa duniani na kesho mbele ya Mungu. Sina cha kukupa wewe kaka, nakuombea kwa Mungu ufanikiwe katika kila jambo unalolifanya!
Hiki ni kisa cha kweli kabisa kama nilivyohadithiwa na yaliyomkuta. Je wewe, mwenzangu, unao uaminifu wa kiasi hicho?
shukurani kwa kaka mrisho abdallah.