JAMANI MAFUA YA KITI MOTO YAPO BONGO
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, leo imetoa tamko juu ya kuingia kwa ugonjwa hatari wa mafua makali ya nguruwe (Swine Influenza/ FLU) hapa nchini.
Wizara hiyo pia imewataka wananchi kuchukua tahadhari kubwa juu ya maambukizi ya ugonjwa huo.
Tamko hilo limekuja kufuatia kubainika kuwepo kwa mgonjwa mmoja ambaye amelazwa katika Hosipitali ya Taifa Muhimbili akiugua ugonjwa huo.
Akitoa tamko hilo katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika wizarani hapo leo , Naibu Waziri katika wizara hiyo Aisha Kigoda, alisema kuwa mgonjwa aliyelazwa Muhimbili ni mwanafunzi , raia wa Uingereza aliyewasili hapa nchini kupitia uwanja wa ndege wa kimataifa wa JK.Nyerere Dar es Salaam, Julai 4, mwaka huu, akitokea London, Uingereza, na ndege ya shirika la Kenya Airways, ambayo ilipitia Nairobi kabla ya kutua Tanzania.
Waziri Kigoda alisema kuwa, mgonjwa huyo ni pamoja na kundi la kwanza la wanafunzi wenzake 15 na walimu wanne. Jumla ya wanafunzi wanaotarajiwa kuja nchini ni 350, kwa ajili ya safari yao ya mafunzo na kupanda mlima Kilimanjaro wakati wa kipindi cha majira ya joto.
Alisema, mgonjwa huyo aligundulika mara moja alipowasili uwanja wa ndege Dar, na kujaza fomu zinazomtambulisha abiria yoyote mwenye dalili za ugonjwa huo.
Aliongeza kuwa mgonjwa huyo baada ya kutua Dar alionekana kuwa na dalili za homa kali, mafua, kuumwa koo, kupiga chafya pamoja na mwili kuwa dhaifu.
Alisema wataalamu wa afya wa uwanja wa ndege, wakishirikiana na wataalamu wa wizara yake makao makuu, walimchukua mgonjwa huyo na kumweka katika chumba maalum na kuchukua sampuli ambazo zilipelekwa maabara iliyopo kwenye Taasisi ya Uchunguzi wa Magonjwa na Binadamu (NIMR) ambapo vipimo vilionesha dhahiri kuwa mwanafunzi huyo alikuwa na vimelea vya mafua makali ya nguruwe.
Waziri Kigoda alisema sampuli zingine zilipelekwa katika maabara inayotambuliwa na Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) iliyopo Nairobi, Kenya, ambapo pia ilithibitika kuwa mwanafunzi huyo ana virusi vya ugonjwa huo.
Alisema mgonjwa huyo alipatiwa matibabu mara moja na kwa sasa amelazwa katika wodi maalum ya magonjwa ya kuambukiza , Muhimbili, ingawa alisema hali ya mgonjwa inaendelea vizuri.
Waziri huyo alidai kuwa uchunguzi pia ulifanywa kwa wanafunzi wenzake na walimu wao na hakuna aliyeonekana kuwa na dalili za ugonjwa huo.
Taarifa za kupiga hodi kwa ugonjwa huo hapa nchini zimeonekana kuwatia hofu wananchi wengi, baada ya vyombo vya habari kuripoti juu ya kuwepo kwa mgonjwa mmoja anayeugua ugonjwa huo.